Jumamosi, 20 Aprili 2013

MBOWE ASEMA SPIKA NI DIKTETA


NI BAADA YA KUHALALISHA UAMUZI WA NDUGAI
KIONGOZI wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amesema kuwa Spika wa Bunge, Anne Makinda analiendesha Bunge kidikteta.
Alisema vurugu na ghasia zinazotokea bungeni wakati wa mijadala mbalimbali zinatokana na spika na naibu wake Job Ndugai kutaka kuliendesha Bunge kidikteta kwa maslahi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alitoa kauli hiyo jana kupinga uamuzi wa spika wa kuridhia adhabu iliyotolewa na Ndugai dhidi ya wabunge sita wa CHADEMA.
Wabunge hao ambao walitolewa bungeni na kuzuiliwa kuhudhuria Bunge kwa siku tano ni Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Ezekiel Wenje (Nyamagana) na Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini).
Awali akisoma uamuzi wake jana bungeni kufuatia mwongozo alioombwa na Mbowe, Spika Makinda alisema uamuzi uliofanywa na naibu wake, Ndugai ni sahihi.
Ndugai aliamuru Lissu atolewe nje kwa kukiuka kanuni ya 60 (12) wakati aking’ang’ania kutoa mwongozo wakati naibu spika akimzuia.
Makinda alisema adhabu hiyo ilitokana na kukaidi agizo la kiti la kumtaka kukaa wakati alipompatia nafasi Mbunge wa Viti Maalumu, Suzan Kiwanga (CHADEMA).
Alisema wabunge wengine watano walipewa adhabu hiyo kwa kosa la kuwazuia wapambe wa Bunge kutekeleza agizo la naibu spika la kutaka kumtoa nje Lissu na kusababisha fujo.
“Waheshimiwa wabunge, kanuni zetu na hasa ya 2 (2) na kanuni ya 5(1) ya kanuni za Bunge imempa mamlaka spika kufanya uamuzi pale ambapo hakuna utaratibu wa kanuni.
“Aidha uamuzi unaofanywa na spika ambao unaruhusu uendeshaji bora wa shughuli za Bunge wa kuleta amani na utulivu bungeni, unaingizwa kwenye kitabu cha maamuzi ili kuongoza mwenendo wa baadaye wa uendeshaji wa Bunge.
“Kwa kitendo kilichotokea Aprili 17 bungeni, hakiwezi kupuuzwa kwa kuwa ni kitendo dhahiri cha kudhalilisha mamlaka ya spika na kilikuwa kitendo cha utovu wa nidhamu wa hali ya juu. Watanzania wote waliushuhudia na wanalaani kilichokuwa kinaendelea ukumbini,” alisema Makinda.
Alifafanua kuwa mbunge yeyote aliyekuwa anaongoza Bunge wakati huo, angeweza kutoa uamuzi huo.
“Ninatumia kanuni ya 5(1) na kanuni ya 2 (2) ya Bunge inayompa mamlaka spika kufanya maamuzi ambapo jambo ama shughuli yoyote haikuwekewa masharti katika kanuni hizi.
“Uamuzi uliofanywa na mheshimiwa Job Ndugai, naibu spika wa kuwatoa nje Mheshimiwa Tundu Lissu…na kubaki nje kwa kutohudhuria vikao vya Bunge siku tano ni halali,” alisema na kuongeza:
“Na sasa utaingizwa katika kitabu cha maamuzi ya spika, na mbunge yeyote atakayefanya vitendo hivi apewe adhabu hii.”

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More