Alhamisi, 11 Aprili 2013

Maddona ashutumiwa na Malawi kutosema ukweli

 
Serikali ya Malawi imemshutumu muimbaji mashuhuri Maddona kwa kutia chumvi kuhusu  kazi yake ya msaada wa kibinadamu nchini humo na kutaka kupewa huduma maalum wakati wa ziara yake nchini humo  wiki iliyopita.

Taarifa kutoka ofisi ya rais Alhamisi  imesema Maddona anataka Malawi iendelee kukaa kwenye kifungo cha kumshukuru kwa sababu amechukua kulea watoto wawili wa Malawi.

Taarifa hiyo imeendelea kutaka kujua nia ya dhati ya kazi yake hiyo ya kusaidia na kusema kwamba muimbaji huyo inabidi ajifunze thamani ya kusema ukweli. Taarifa hiyo imesema amechangia ujenzi wa madarasa na sio kujenga shule kama ilivyodaiwa .

Madonna naye kwa upande wake amesema amesikitishwa na rais wa Malawi Joyce Banda ambaye amechagua kudanganya juu ya kazi zake za misaada , nia yake na jinsi alivyofanya wakati alipokuwa nchini humo.

Taarifa kwenye mtandao wake wa Raising Malawi inasema Madonna hapo awali alitaka kujenga shule ya wasichana lakini akagundua kwamba lengo lenye maendeleo  zaidi litakuwa ni kujenga shule ndogo ndogo katika vijiji nchini kote.
Maddona anasema kutokukubaliana kwao kumetokana na kufukuzwa kazi kwa dada wa rais Banda , Anjimile Oponyo ambaye alifanya kazi kama mkuu wa taasisi hiyo ya misaada. Oponyo alifukuzwa kazi kufuatia shutuma za matumizi mabaya ya dola milioni 3.8 za misaada.

Oponyo anashitaki taasisi hiyo kwa kumfukuza kazi kimakosa.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More