Jumapili, 21 Aprili 2013

Lipumba: Kipato cha mkazi Dar 640/-


MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema theluthi tatu ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanakabiliwa na umasikini wa kutisha kutokana na kuishi kwa kipato cha sh 640 kwa siku.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Lipumba alisema kongamano la kujadili maendeleo ya Mkoa wa Dar es Salaam limeandaliwa na chama chake, Taasisi ya Demokrasia ya Denmark huku washiriki 130 wakitoka taasisi za serikali, viongozi wa dini na mashirika.
Lipumba alisema chimbuko la umasikini huo limechangiwa na ongezeko la watu huku wengi wao wakikabiliwa na ukosefu wa ajira za kueleweka.
Alisema jiji hilo lina idadi ya wakazi wapatao milioni 4.5, kati yao milioni 1.3 ndiyo wenye ajira na wengine ajira zao ni za kubahatisha.
“Haiingii akilini kwa maisha ya jiji la Dar es Salaam mtu aweze kuishi kwa sh 640, hii si kweli, wote tunajua maisha ya jiji hili yalivyo,” alisema.
Katika kupunguza tatizo la ajira, Lipumba alisema mikakati ya makusudi ya kuanzisha viwanda ambavyo vitachechemua uchumi inatakiwa haraka.
Alivitaja baadhi ya viwanda hivyo kuwa ni vya ngozi, mavazi, umeme, viatu na vingine ambapo alitahadharisha kuwa kusiwe na urasimu kwa watu watakaojitokeza kwa ajili ya kutaka kuvianzisha.
Aidha, Lipumba alisema sekta ya elimu bado inakabiliwa na changamoto lukuki ambazo zinahitaji mjadala mpana utakaosaidia kuupatia ufumbuzi wa kudumu.
Alisema bila ya kuwa na elimu bora ambayo itazalisha wataalamu mbalimbali wakiwemo wa sayansi, nchi hii haiwezi kusonga mbele kimaendeleo.
“Na hii elimu yetu bado inakabiliwa na matatizo kutokana na watoto wetu kufundishwa lugha ya Kiswahili na wanapofika sekondari lugha inayotumika ni Kingereza hali inayowafanya wafeli mitihani yao,” alisema.
Lipumba alisema ukiachilia mbali wanafunzi hao kushindwa matumizi ya Kingereza bado wapo ambao wanamaliza elimu ya msingi hawajui kusoma vitabu vya Kiswahili.
Baadhi ya washiriki kwa nyakati tofauti walisema ukusanyaji wa makato katika halmashauri bado hauridhishi, wakati mwingine yanayokusanywa ni asilimia 40 lakini mipango yake inazidi ya kawaida kwa asilimia 70.
Mratibu wa kongamano na Taasisi ya Vyama na Demokrasia (DIPD), Anemon Birkebaek alisema atatumia uzoefu wake kuwaunganisha vijana wa Denmark na wa hapa nchini ili waweze kubadilishana uzoefu katika kujiletea maendeleo.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More