Alhamisi, 11 Aprili 2013

Mfadhili wa Odinga akamatwa na Sh bilioni 6

ALIYEKUWA mfadhili wa mgombea urais wa Kenya, Raila Odinga ambaye pia aligombea ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, Donbosco Gichana (34), amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kutakatisha fedha haramu zaidi ya Sh bilioni sita.

Gichana alipanda kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru.

Akisoma mashtaka hayo, Wakili wa Serikali, Osward Tibabyekomya akisaidiwa na Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka alidai mshtakiwa anakabiliwa na mashtaka mawili.

Osward alidai katika shtaka la kwanza, inadaiwa akiwa na washtakiwa wengine ambao hawapo mahakamani kati ya Novemba 2009 na Agosti 2010 jijini Nairobi, Kenya, Arusha na Dar es Salaam walikula njama ya kutakatisha fedha haramu.

Wakili wa mshtakiwa huyo, Semu Anney alidai mteja wake alikuwa mfadhili mkuu wa Raila Odinga katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007, nchini Kenya na ndiye aliyempa gari aina ya Hammer kwa ajili ya kufanyia kampeni wakati huo.

Inadaiwa mshtakiwa alifanya kosa hilo kinyume cha kifungu namba 12 cha sheria ya kuzuia utakatishaji fedha haramu namba 12 ya mwaka 2006.

"Mheshimiwa shtaka la pili, anashtakiwa kwa kutakatisha fedha haramu, inadaiwa kati ya Novemba 2009 na Agosti 2010 kwa kupotosha ukweli wa chanzo cha fedha alizokuwa nazo, alizihamisha kutoka Kenya kwenda Arusha na Dar es Salaam.

"Anadaiwa kuhamisha fedha kwa kutumia hundi yenye thamani ya Dola za Marekani 4,940,363.25 na kuziweka katika akaunti namba 02J1036325000 inayomilikiwa na Moyale Precious Germs Enterprises iliyopo Benki ya CRDB tawi la Meru Arusha.

"Mshtakiwa alihamisha tena fedha hizo kutoka tawi la Meru Arusha, kwenda makao makuu ya benki ya CRDB Dar es Salaam, kwa nia ya kufanya utaratibu wa kuzitoa wakati akijua hundi ilikuwa ya kughushi," alidai Osward.

Hakimu Mchauru, alimfahamisha mshtakiwa kwamba hatakiwi kujibu lolote, kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na aliahirisha kesi hadi Aprili 18 mwaka huu.

"Gichana pamoja na kuwa mfadhili wa Odinga, pia aligombea ubunge Jimbo la Kisii kwa tiketi ya ODM, Kenya lakini hakupata ushindi, mwaka huu hakumfadhili kwa sababu na yeye alikuwa mgombea," alidai Wakili Anney.

Uchaguzi Mkuu wa Kenya ulifanyika Machi 4, mwaka huu na Odinga alishindwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alishinda kwa tofauti ya kura 800,000.

Kenyatta aliapishwa juzi na Msajili Mkuu, Gladys Sholei mjini Nairobi ambapo Odinga inadaiwa alikimbilia Afrika Kusini.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More