Jumatano, 17 Aprili 2013

MTOTO WA MKULIMA, Pinda na Sh1 bilioni ya mazishi

Ombi hilo la Waziri Mkuu limekuja wakati kukiwa na vilio vya ukosefu wa huduma bora za jamii huku maisha ya Watanzania yakidorora.
Akiwasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka 2013/2014, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya Sh123 bilioni (123, 401,059,000) kwa ajili ya Mfuko wa Bunge na Sh4 trilioni nne, (4,226,123,954,802) kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Waziri Mkuu – Tamisemi ikiwa ni matumizi ya kawaida na fedha za maendeleo za ndani na nje, ambapo kati yake ameomba kiasi cha Sh1 bilioni kwa ajili ya mazishi ya viongozi.
Ombi hilo la Waziri Mkuu limekuja wakati kukiwa na vilio vya ukosefu wa huduma bora za jamii kama afya, chakula, maji na hali za maisha ya Watanzania zikiendelea kudorora.
Wakichangia mjadala wa bajeti hiyo baadhi ya wabunge na wanasiasa wameguswa na kuhoji vigezo vilivyotumika kutenga kiasi kikubwa hicho cha pesa kwa ajili ya mazishi ya watu walio hai badala ya kutumia kiasi hicho cha pesa kurekebisha huduma bora za wananchi ili kuwaondoa katika hatari za kupoteza maisha.
Mbunge wa Viti Maalumu wa Chadema, Lucy Owenya ndiye aliyeibua hoja hiyo wakati akichangia hotuba ya makadirio na matumizi ya ofisi hiyo iliyowasilishwa bungeni na Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliposema inashangaza kutenga mabilioni kwa watu watakaokufa badala ya kuwekeza fedha hizo kwa maendeleo ya walio hai.
Anasema Katika hali inayotafsiriwa kuwa ni ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma, Serikali inawajali viongozi watakaokufa na kupuuza kufutatua matatizo ya akina mama wajawazito wanaolala chini au wanne kitanda kimoja katika hospitali nyingi nchini.
Owenya akaitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kupunguza fedha hizo na kuzitumia  kujenga chumba cha upasuaji cha hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi pamoja na kuisaidia Hospitali Teule ya St Joseph kununua vitanda vya wodi ya wazazi.
“Ni aibu na fedheha kubwa kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya maandalizi ya kuzika viongozi, huku mambo muhimu na ambayo ni kipaumbele yakiachwa, hivi mmetenga kiasi hicho kwani mnajua nani atakufa na lini atakufa ndiyo mnajiandaa kumzika, ni aibu kutenga kiasi kikubwa hiki cha pesa kwa ajili ya watu watakaokufa na ambao kwa sasa wapo hai…Kwa nini pesa hii isitumike kwa maendeleo ya watu waliohai,” anahoji Owenya.
Mbunge huyo akaongeza kusema Serikali imeshindwa kufikiri hasa namna ya kuwaondolea umaskini na taabu wanazopata wananchi wake lakini inathibutu kutenga kiasi kukubwa cha fedha kwa ajili ya kuwazika viongozi ambao bado wapo hai.
Mbunge mwingine aliyeonyesha kukerwa na bajeti hiyo iliyosomwa na Waziri Mkuu ni Kangi Lugola wa Jimbo la Mwibara (CCM) anayesema licha ya kuwa mbunge wa CCM haungi mkono bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa kile aliochosema kitendo cha kutengea Sh1 bilioni kwa ajili ya mazishi ya viongozi watakaokufa ni ubadhirifu.
Lugola ameongeza kuwa hataunga mkono bajeti hiyo kwa sababu hajui atakufa lini.
“Mazishi gani ya viongozi kwa shilingi bilioni moja? Huu ni wizi mtupu ndani ya Serikali, kama wasipokufa tutapata ripoti ya matumizi mengine ya fedha hizo? Siungi mkono hoja mpaka nione bajeti inaeleza mikakati na dhamira ya dhati ya kumaliza rushwa na dawa za kulevya nchini,” anasema.
Mbali na wabunge hao, wanasiasa wengine wamezungumzia bajeti hiyo ya Waziri Mkuu na kusema Serikali inapaswa kuwa makini na matumizi ya pesa za wananchi na kuzitumia kwa manufaa ya maendeleo yao na siyo ya kundi dogo la viongozi.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More