CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeibua tuhuma nzito za ufisadi wa mabilioni ya fedha, kikidai kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), hasa kupitia makundi ya wasaka urais, kimeanza kutumia mbinu haramu kutafuna fedha za Watanzania kwa ajili ya kampeni za 2015, kwa namna ile ile iliyotumika kufanikisha wizi wa EPA, wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2005.
Katika mkutano na waandishi wa habari, CHADEMA kimedai kuwa ufisadi huo
unasimamiwa na Waziri wa Uchukuzi, Harrison Mwakyembe, kikimtuhumu kuwa
anatumia madaraka yake ya uwaziri ‘kuipatia’ Kampuni ya CCM iitwayo
Jitegemee Trading Company zabuni ya kujenga mradi yenye thamani ya
bilioni 10, kinyume cha taratibu kujenga eneo la maegesho kwenye eneo la
CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa
Oganaizesheni na Mafunzo wa CHADEMA, Singo Benson Kigaila, amesema kuwa
kwa msukumo wa Mwakyembe, Mamlaka ya Bandari (TPA), imetoa zabuni kwa
kampuni hiyo inayodaiwa ni ya CCM, kujenga maegesho ya magari makubwa,
makontena na malori eneo la SUKITA (Tabata) jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa kwa mujibu wa nyaraka ambazo chama hicho kimezinasa,
Kampuni ya Jitegemee imepewa zabuni hiyo kinyume na shera za nchi,
hususan ile ya Manunuzi ya Umma (PPRA), akisisitiza kuwa hakuna zabuni
yoyote iliyotangazwa ili kuruhusu ushindani wa makampuni mbalimbali
yenye sifa kufanya kazi hiyo.
“Ndugu wanahabari, mchezo wanaofanya CCM, hasa kupitia magenge ya
watafuta urais, ni ule ule kutumia makampuni yao, mengine yakiwa hewa,
kutafuta fedha haramu kwa kuwaibia Watanzania kama walivyofanya kabla na
wakati wa uchaguzi wa mwaka 2005, pale makampuni yao yalipoiba fedha
Benki Kuu na kusaidia kampeni za CCM kumpeleka Kikwete ikulu.” Alisema
Benson na kuongeza;
“Sasa wameanza tena…wameanza kwa kupitia kampuni yao iitway Jitegemee
Trading Company. Watalipwa bilioni 10, tena tayari zimeshapangwa kwenye
bajeti ijayo. Kampuni hii kwa msukumo wa Mwakyembe, imepewa zabuni ya
ujenzi wa maegesho eneo la SUKITA, yaani kampuni ya CCM imepewa zabuni
kinyemela, kujenga maegesho kwenye eneo la CCM…kama mnavyojua eneo hilo
lililopo Tabata, ni mali ya chama hicho.
“Kuna hoja tano za msingi hapa; kwanza mradi huu unaotaka kufanywa na
Mwakyembe kwa kutumia kivuli cha TPA, kampuni hiyo haijafanyiwa tathmini
ya upembuzi yakinifu…sawa sawa tuna ilivyokuwa kwa Kampuni ya kitapeli
ya Richmond ambayo Mwakyembe huyo huyo akisoma ripoti yake bungeni
alisema ni kosa.
“Pili, mradi hu wa Mwakyembe na chama chake, haukufuata Sheria ya
Manunuzi ya Umma. Hakukuwa na zabuni iliyotangazwa wala ushindani kwa
makampuni mengine yenye sifa kushindana. Tatu; nyaraka zilizopo TPA
zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2010 Bodi ya Bandari ilipokea maombi kutoka
Manispaa ya Temeke ya kutaka kufanya ubia wa eneo la maegesho huko
Kurasini
“Wazo hili halijawahi kufanyiwa kazi badala yake Mwakyembe amekuja na
mradi wake. Vyanzo vyetu ndani ya serikali na CCM vinasema kuwa mmoja wa
wajumbe wa TPA alipohoji kwa nini shirika linaingiza feha hizo kwenye
mradi huueneo la SUKITA, Mkurugenzi wa Bandari alijibu “huuni mradi wa
chama tawala, hivyo ni muhimu tukau-support,” alisema Kigaila akinukuu
kikao cha bodi ya bandari.
Aliongezea akisema kuwa jambo la jingine katika mradi huo aliouita ni
ufisadi wa kuitafutia CCM fedha kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mkuu wa
2015 na ule wa serikali za mitaa mwaka ujao, ni uamuzi wa serikali
kwenda kujenga mradi mkubwa kama huo eneo la Bonde la Msimbazi.
“Kila siku wanawaambia Watanzania wahame mabondeni…leo wanapeleka
kujenga mradi huu eneo la bondeni ambako CCM walikuwa wakitumia kufuga
ng’ombe na nguruwe na wakasombwa na mafuriko. Sasa leo wanataka magari
makubwa, malori na makotena, mali za wateja ziengeshwe pale.
“Mbali na mradi huu kuitafutia CCM na genge la watu wengine wasaka
urais fedha haramu kwa mgongo wa kodi za walipa kodi, mradi huu
utasababisha hasara kubwa huko mbeleni, hasa pale mvua kubwa
zitakapoanza kusomba mali za wateja…kumbukeni Mwakyembe yuko kwenye
genge moja la urais na Samuel Sitta, Bernard Membe, anayeungwa mkono na
Kikwete,” alisema Benson.
Mkurugenzi huyo wa Oganazisheni na Mafunzo wa CHADEMA alisema kuwa
tangu Mwakyembe aondoe uongozi wa zamani wa Mamlaka ya Bandari, yeye na
viongozi wapya, wamepuuza miradi yote ya mwanzo na badala yake
wameingiza miradi mipya takriban 35, ambayo imeombewa fedha kwa nia hiyo
hiyo ya kusaka fedha za urais.
Amewataka Watanzania kuzijua sura mbili za Waziri Mwakyembe, akidai
kuwa si kiongozi wa kuaminika, akikumbushia namna alivyolinda maslahi ya
CCM kwa kuwaficha Watanzania baadhi ya masuala katika kashfa ya
Richmond na kukaa kimya pale maazimio ya bunge yaliyotokana na kamati
yake, yalipopuuzwa.
Mwakyembe ndiye alifanikisha kujiuzulu kwa aliyekua Waziri Mkuu, Edward
Lowassa,baada ya kuuvalia njuga mradi wa kifisadi ulopewa kampuni ya
Richmond Development LLC, kwa njia ambayo sasa anautoa kwa kampuni ya
Jitegemee.
Hatua hiyo ilimpa heshima kubwa Mwakyembe, jambo ambalo wadadisi wa
mambo wamesema sasa ametumia heshima hiyo "kufanya atakavyo" hata
kufikia hatua ya kuingia kwenye ufisadi.
0 maoni:
Chapisha Maoni