Korea Kaskazini imehamisha makombora mengine kwenye mwambao wake wa Mashariki tayari kwa mashambulizi dhidi ya Marekani, huku nchi hiyo inayotishiwa kushambuliwa ikisema inachukua tahadhari kutokana na vitisho hivyo.
Kulingana na chombo cha habari cha Yonhap cha Korea Kaskazini kikimnukuu
afisa mmoja wa serikali nchini humo, makombora mawili tayari
yameshasafirishwa kwa treni mapema wiki hii na kuwekwa katika magari
tayari kwa kushambulia.
Kwa upande wake Wizara ya ulinzi ambayo ilithibitisha kupelekwa kwa
kombora la kwanza ilikataa kutoa maoni yake juu ya habari za hivi
karibuni kwamba makombora mengine yamesafirishwa Mashariki mwa pwani ya
nchi hiyo.
Hata hivyo afisa mmoja wa jeshi amekiambia chombo hicho cha
Yonhap kwamba, makombora yaliyosafirishwa yametegeshwa Mashariki na
Magharibi mwa pwani ya Korea Kaskazini.
Vitisho hivyo vya Korea kaskazini ni mojawapo ya misururu ya vitisho vya
wiki kadhaa sasa, kufuatia vikwazo vya Umoja Wa Mataifa dhidi yake na
mazoezi ya pamoja ya kijeshi kati ya Marekani na Korea kusini.
Marekani yatoa maoni yake
Huku hayo yakiarifiwa Marekani imesema itaweka mizinga ya kujikinga na
makombora katika kisiwa chake cha Pasifiki cha Guam kuimarisha uwepo
wake wa kijeshi katika eneo hilo.
Hata hivyo wachambuzi wengi wanaofuatilia swala hili kwa makini wanasema Korea Kaskazini haina uwezo wa kuishambulia Marekani.
Waziri wa ulinzi wa Marekani, Chuck Hagel, amesema vitisho
vinavyotolewa na Pyongyang vinatia hofu kwa taifa hilo zima na hata
washirika wake kama Korea Kusini na Japan.
Tangu vitisho kuanza kutolewa kumekuwa na fununu kwamba mashambulizi
hayo huenda yakafanyika siku ya kuzaliwa kwa kiongozi wa zamani wa nchi
hiyo, hayati Kim Il-Sung, ambayo ni katikati ya mwezi wa Aprili.
Ban Ki Moon aisihi Korea Kaskazini kusimamisha vitisho
Vitisho hivyo vya mara kwa mara kutoka Korea Kaskazini kwa Marekani vimezua hisia mbali mbali miongoni mwa jamii ya kimataifa.
Kwa upande wake katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, akisema
kwamba vitisho vya aina hiyo vinatia hofu na huenda vikasababisha athari
kubwa.
"Nadhani wamekwenda mbali katika vitisho vyao, na nina wasi
wasi kwamba iwapo ghasia hizo zitatokea katika rasi ya Korea basi swala
hili litakuwa na athari kubwa sana," Alisema Ban Ki Moon.
Hapo jana Korea kaskazini iliwazuia wafanyikazi kutoka Korea kusini
kuingia katika kiwanda cha Keosong. Hatua hiyo inalenga kuwasimamisha
kazi wafanyakazi takriban 53,000 kutoka Korea Kusini.
0 maoni:
Chapisha Maoni