Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ameiponda Serikali kwa kuwa
na uchumi unaokua kwenye makaratasi wakati maisha ya wananchi
yakiendelea kuwa magumu siku hadi siku.
Akizungumza mbele ya
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Bilal, Profesa Lipumba alisema uchumi wa
Tanzania hivi sasa unakwenda kama mtoto anayetambaa akiwa na watu wazima
wanaokimbia.
“Tulikuwa na mipango
mingi lakini isiyotekelezeka, tulielezwa ni lazima tukimbie wakati
wenzetu wanatembea, lakini badala ya kuongeza mbio, sasa tunatambaa
wakati nchi za wenzetu zinakimbia kwa kasi kimaendeleo,” alisema Profesa
Lipumba.
Alisema ingawa uchumi
unakua kwa asilimia saba kwa mwaka, lakini ukuaji huo haulingani na
maisha ya wananchi ambayo yanazidi kuwa magumu siku hadi siku.
Profesa
Lipumba ambaye kitaaluma ni mchumi, alisema sekta ya kilimo ambayo
inaajiri asilimia 75 ya wananchi inakuwa kwa asilimia 25.
“Unategemea nini kama
sekta ambayo inawahusisha wananchi wengi, lakini bado haijaboreshwa ili
iwanufaishe,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema ingawa Serikali
imekuwa na mipango mizuri, lakini imeshindwa kuitekeleza hatua ambayo
inawafanya wananchi wakate tamaa ya maisha.
Akitoa mfano, alisema kitendo cha kuwa na vipaumbele vingi wakati uwezo wa fedha ni mdogo ni kikwazo cha kuleta maendeleo.
“Hata kwenye bajeti zetu
tumekuwa na vipaumbele vingi kiasi kwamba hata kuvitekeleza inakuwa
vigumu, tuchague vipaumbele vichache na tuvifanyie kazi,” alisema
Profesa Lipumba.
Kwa upande wake, Makamu
wa Rais, Dk Bilal alisema kukua kwa uchumi unaowafikia wananchi ni
mchakato ambao hauwezi kuja ghafla. Alisema kitendo cha Serikali
kutengeneza miundombinu ikiwamo barabara ni moja ya juhudi zinazofanywa
ili wananchi waweze kunufaika.
“ Ni kweli ukuaji wa
uchumi haufanani na maisha ya wananchi wengi, lakini hatua
zinazochukuliwa na Serikali kama kujenga barabara, maji ,huduma za afya
na elimu zinasaidia kukuza uchumi kwa watu walio wengi,” alisema Dk
Bilal.
Naye,Mkurugenzi Mtendaji
wa Repoa, Profesa Samwel Wangwe alisema mkutano huo wa watafiti
unaangalia namna ukuaji wa uchumi na maisha ya wananchi walio wengi.
Kwa upande wake,Mtaalamu
wa masuala ya uchumi kutoka Malaysia, Datuk Chris Tan alisema uchumi
utakuwa juu kama viongozi watakuwa na nia ya dhati ya kuleta mabadiliko.
0 maoni:
Chapisha Maoni