Hoja ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi iliibuliwa bungeni kwa mara
ya kwanza na Augustine Mrema, wakati huo akiwa mbunge kwa tiketi ya
NCCR-Mageuzi, lakini Bunge liliibeza, halikuijadili na hivyo likafa.
Baadaye lilfufuliwa na Thomas Ngawaiya, wakati huo akiwa mbunge kwa
tiketi ya Chama cha Tanganyika Labour Party (TLP), huku Mrema akiwa
Mwenyekiti wa chama hicho, na taratibu ikaanza kushika mwendo miongoni
mwa Waislamu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2000.
Kwa hofu ya kupokonywa kura za Waislam na upinzani, Chama Tawala,
CCM, kiliidaka hoja hiyo na kuifinyangafinyanga na hatimaye kuingizwa
katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM kwa mtindo wa ‘funika kombe mwanaharamu
apite.’
Mrema na Ngawaiya wote ni Wakristo, na Mahakama ya Kadhi ni kwa
Waislamu pekee. Hivi pilipili ya shamba wasiyoila iliwawashia nini hawa
wawili, kama si uzandiki wa kisiasa kwa lengo la kujipatia umaarufu na
kura za jamii ya Kiislamu?
Nacho CCM, hali kikijua kuwa hoja hiyo ilikuwa ni ya kibaguzi na
kinyume cha Katiba ya nchi; kwanini kiliudanganya umma ‘kufunika kombe’
wakati kikifahamu kuwa hatua hiyo ilikuwa hatari kwa mustakabali wa nchi
na kwa umoja wa kitaifa?
Duniani kote, wasababishao vita ni Wanasiasa ambao daima wana tabia
chafu ya kusema wasichoamini, na kuamini wasichosema. Kwa mchezo huu
mchafu wa kisiasa, CCM ikawa imejitia kitanzi, na hadi sasa bado
inamung’unya maneno suala la Mahakama ya Kadhi linapotajwa. Kwa nini? Ni
uzandiki tu!
Kinjekitile Ngwale, yule ‘mganga’ wa Vita ya Maji Maji, alisema
asichoamini kwa kuwaambia watu wake wenye silaha duni, wapigane na
Wajerumani wenye silaha kali za moto, kwa madai kuwa risasi za Wazungu
hao zingegeuka maji zisiweze kuwadhuru.
Kwa kumwamini, Wamatumbi hao walithubutu, lakini wakateketezwa kwa
risasi kwa maelfu, katika vita iliyokuja kujulikana kama Vita ya Maji
Maji. Kinjekitile, licha ya kujutia uongo wake, lakini alikuwa
amesababisha maafa makubwa kwa jamii kwa ulimi wake. Lakini wanasiasa
wetu, tofauti na Kinjekitile, si watu wastaarabu, hawajui kujutia
ulaghai wao, wala kuomba samahani kwa wanaodai kuwaongoza.
Itakumbukwa kwamba wakati Fulani, hoja hiyo ilipopamba moto na
Serikali ikijiuma midomo isijue la kunena, kiasi cha Baraza la Maaskofu
nchini (TEC) nalo likaandaa rasimu yake ya kutaka itungwe sheria ya
kuanzisha Mahakama ya Kikristo kwa kuzingatia hali ya maisha ya waumini
wake na kugharamiwa na Serikali, kama wanavyodai tu watetezi wa Mahakama
ya Kadhi.
Na vivyo hivyo, wafuasi wa dini za jadi walianza nao kufikiria
kurudishiwa tawala za Watemi waweze kurejeshewa Mahakama zao za jadi,
kwa kuzingatia mfumo na hali ya maisha yao. Madai ya TEC na ya watetezi
wa jadi yangali hai bado, na bila shaka yoyote yataibuka hima pindi
Mahakama ya Kadhi ikipendelewa na kwa umma kubebeshwa mzigo wa
kuigharamia.
Bila shaka kesho na kesho kutwa Mabohara, Wahindu, Wabudha na vikundi
vingine vyenye imani mbalimbali navyo vitataka Mahakama zake. Ubaguzi
huu utalipeleka wapi Taifa letu hili huku tukitizama tu kwa
‘kuwaheshimu’ wanasiasa uchwara na wazandiki kwenye nchi inayodai haina
dini, bali watu wake?
Isingekuwa uzandiki wa wanasiasa uchwara, nchi yetu haikuwa na tatizo
juu ya taasisi za kidini zilizowekwa na wakoloni wa Kiingereza kwa
lengo la kuwagawa wazalendo ili iwe rahisi kuwatawala chini ya mfumo
uliobuniwa na gwiji la ukoloni barani Afrika, Kapteni Frederick D.
Lugard, ujulikanao kama ‘Lugardian Indirect Policies,’ ambapo Nigeria na
Uganda ziliteuliwa nchi za mfano barani Afrika.
Mfumo huo, ambao unajulikana pia kama ‘divide and rule’(D&R),
unajieleza vizuri katika kitabu cha Lugard kiitwacho ‘Dual Mandate’
kilichochapishwa mwaka 1929. Huo ndiyo mfumo unaotusumbua hadi sasa
tunapoendeleza ukabila, udini, ukanda, itikadi za vyama, uanamitandao na
dhambi nyingine za kibaguzi kwa gharama ya umoja wa kitaifa na
uzalendo.
Kufufuliwa kwa hoja ya Mahakama ya Kadhi, ni hatua moja ya kufufua
sera za Lugard. Tanganyika ilikuwa na Mahakama ya Kadhi na Mahakama
nyinginezo kabla na baada ya Uhuru, hadi mwaka 1963 zilipofutwa.
Mahakama ya Kadhi inaanzishwa kwa ajili ya kuamua au kuhukumu mashauri
yanayohusu jamii ya Kiislamu pekee kwa kutumia sheria zao, maarufu kama
Shariah; na kwa nchi zenye mfumo huo zisizo za kisekulari, kwa maana ya
mamlaka ya nchi kuongozwa kwa misingi ya dini tawala (dominant
religion), Mahakama za Kadhi na Ofisi ya Kadhi hugharamiwa na Serikali.
Kutimiza yote haya, wakoloni waliweka mfumo wa sheria msonge wenye
ngazi tatu (a three tier legal pyramid). Kwenye kilele cha mfumo huo,
kulikuwa na sheria asilia za Uingereza (British Common Law) zilizokuwa
na nguvu turufu juu ya migogoro kati ya mtawala na mtawaliwa.
Chini ya sheria hizo, kulikuwa na sheria za Kiislamu (Islamic Laws)
kwa nchi zilizokuwa na idadi kubwa ya Waislamu. Mfano ni huko Nigeria ya
Kaskazini ambako Ufalme wa Sokoto, uligawanywa katika majimbo na
kuruhusiwa kuundwa katika majimbo Mahakama za Kiislamu chini ya Kadhi
Mkuu, kama ilivyo Zanzibar hivi sasa.
Ingawa mpaka sasa Nigeria inajiita taifa lisilo na dini (a secular
state), mifarakano ya mara kwa mara iletwayo na waumini wa dini ya
Kiislamu dhidi ya waumini wa dini nyingine, inaonyesha namna dini hiyo
inavyoongoza na kutawala siasa za nchi hiyo. Mifarakano kwa misingi ya
kidini, ilikuwa chanzo pia cha vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1967,
maarufu kama ‘Vita ya Biafra.’
Chini ya msonge huo wa sheria, kulikuwapo mfumo wa sheria za jadi
(Customary Legal System) za Afrika ya kale zilizotambua nguvu za
watawala wa jadi (Watemi) na ziliwahusu Waafrika ambao hawakutaka
kufungwa nira na sheria za Kiislamu au zile za Kimagharibi.
Kulikuwa na Mahakama Kuu na Mahakama nyinginezo (Subordinate Courts)
kwa mujibu wa sheria ya Mahakama ya 1920. Mahakama za wenyeji (Native
Courts) ziliundwa chini ya kifungu cha 3 (4) cha sheria hiyo, na
ziliwagawa Watanganyika kwa kuweka Mahakama ya Liwali, Mahakama ya
Kadhi, Mahakama ya Akida, Mahakama ya Mtemi, Mahakama ya Mwanangwa
(Headman) au mtu mwingine yeyote atakayepewa na Gavana uwezo wa Mahakama
za Wenyeji.
Oktoba 1961, aliyekuwa Waziri wa Sheria wakati huo, Alhaji Chifu
Abdallah Fundikira (Mwislamu), aliwasilisha bungeni Muswada wa kubadili
mfumo wa Mahakama mbili; Mahakama Kuu na Mahakama za Wenyeji ndani ya
nchi moja (Tanganyika) kwa lengo la kujenga umoja wa kitaifa ili kupiga
vita ubaguzi wa aina yoyote katika utoaji haki mbele ya sheria.
Mabadiliko hayo yalifikia kilele mwaka 1963 kwa kupitishwa sheria ya
Mahakama (Magistrates Court Act) Namba 55, iliyounganisha Mahakama za
Wenyeji na Mahakama zilizokuwa chini ya Mahakama Kuu, na kufanya nchi
kuwa na mfumo mmoja tu wa Mahakama, ambao Jaji Mkuu wa Kwanza wa
Tanganyika, Telford Georges, aliusifia kuwa ni mfumo makini, rahisi na
wazi kuliko mifumo yote ya Mahakama Afrika Mashariki, kama si Afrika
nzima.
Mfumo huo ndio ulioanzisha Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya na
Mahakama ya Hakimu Mkazi, na kuweka taratibu za rufaa kutoka Mahakama
hizo. Licha ya kufutwa tena kwa sheria hiyo, na nafasi yake kuchukuliwa
na sheria ya Mahakama ya Mwaka 1984, mfumo wetu wa Mahakama unabakia ule
ule wa mwaka 1963 ambao hauna ubaguzi katika utoaji haki.
Kubadilika kwa mfumo wa Mahakama baada ya Uhuru, hakukuwa na maana
kwamba migogoro au masuala yaliyokuwa yakishughulikiwa na Mahakama za
Kadhi na nyinginezo haina taasisi za kuisuluhisha. Waislamu, Wakristo na
Wenyeji hawazuiwi kuunda mabaraza na taratibu zao za kusuluhishana,
bila kuhusisha mamlaka ya nchi.
Mahakama zetu zimepewa uwezo wa kusikiliza na kuamua kwa haki bila ya
ubaguzi, mashauri yote kwa kuzingatia sheria yoyote inayomhusu mtu au
mlalamikaji, pamoja na mashauri yanayohusu mikataba halali na huru kwa
matakwa ya wanamkataba. Ukiondoa jazba za kisiasa, jazba za kidini
(tajdeed) na agenda nyingine za siri, kama taifa, hatuna matatizo na
mfumo huo.
Je; iwapo mambo haya yataachwa kuendeshwa kwa misingi ya kidini, kwa
upendeleo na kwa gharama ya Serikali, tuna hakika gani kesho taasisi
hiyo haitaendelea kudai mfumo mpya wa kidini kuhusu elimu, sayansi na
teknolojia, mabenki, bima au uhusiano wa kimataifa ili kukidhi matakwa
ya sehemu moja ya jamii kwa misingi ya dini katika taifa?
Tabaka kwa misingi ya dini zinaporuhusiwa kujitokeza katika jamii,
huleta mifarakano na mitafaruku inayoweza kutishia usitawi wa jamii
kwani mara nyingi tabaka kama hizi, huwa na agenda ya siri. Ni chui
ndani ya ngozi ya kondoo. Yaliwahi kutokea huko Algeria chini ya chama
cha kutetea harakati za Kiislamu cha FLS, ambapo Serikali ya nchi hiyo
iliondolewa madarakani kwa nguvu ya ‘Tajdeed’ au ‘Uamsho’ wa Kiislamu
(Islamic Revivalism).
Vivyo hivyo, ilitokea huko India mwaka 1993, ambapo chama cha siasa
cha BJP kilipenyeza agenda yake ya siri, kwa kuamsha hisia za kidini
chini ya dhana ya ‘Uamsho’ juu ya utukufu na heshima ya dini ya Kihindu
iliyodaiwa kupotea miongoni mwa waumini milioni 730 wa dini hiyo, katika
taifa lenye Waislamu wapatao milioni 110 tu.
Kwa hiyo, ‘Uamsho’ wa kidini mara nyingi una agenda mbili kuu; mosi
ni agenda ya kidini na pili, ni agenda ya kisiasa. Tukubali, tusikubali.
Watanzania hawawezi kuyumbishwa na agenda za siri za baadhi ya
wanasiasa wachovu wanaotaka kuturejesha kwenye enzi za utawala wa kina
Frederick Lugard.
Tunawashukuru Wazanzibari, chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa,
kuiondolea taasisi ya ‘Mahakama ya Kadhi’ hadhi ya Kikatiba, tofauti na
wahafidhina wanaoshinikiza iwe kwenye Katiba ya Muungano, baada ya
kufutwa kwa ibara ya 98 ya Katiba ya Zanzibar kufuatia marekebisho ya
2010, kwamba Katiba hiyo sasa haina msamiati huo tena. Kwa sababu hii,
inaweza kusema kuwa sheria ya Mahakama ya Kadhi Na. 3 ya mwaka 1985,
inahojika chini ya Katiba yao.
Wala jamii yetu haiwezi kukubali kugawanywa kwa misingi ya kidini
kuturejesha enzi za vita vya kidini vya karne ya 14, kati ya Wakristo na
Waislam. Waswahili walisema bila kukosea; kwamba ukimruhusu ngamia
kuingiza kichwa hemani, muda si muda atataka kuingia mwili mzima; na
akifanya hivyo, elewa hema lako liko hatarini kuwa vipande vipande.
Source: raia mwema
Source: raia mwema
0 maoni:
Chapisha Maoni