Alhamisi, 16 Mei 2013

Askofu Mtega wa jimbo kuu la kanisa katoliki Songea ajiuzulu

KIONGOZI Mkuu wa jimbo Kuu la Kanisa Katoliki Songea , Mhashamu Askofu Norbeth Mtega amejizulu. Taarifa za kujiuzulu kwa kiongozi huyo zilipatikana jana saa saba mchana zikieleza kuwa Askofu Mtega alikuwa ametembelea Abasia ya Wabeneditini iliyopo Hanga wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma.
Mhashamu Askofu Mtega alipokuwa katika abasia hiyo ya Hanga aliwatangazia waumini na watawa wa Shirika la Wabeneditini kuwa kuanzia sasa yeye siyo Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea.

Alisema badala yake jimbo hilo litashikiliwa na Askofu wa jimbo la Iringa, Taricisius Ngalalekumtwa ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza la maskofu Tanzania mpaka atakapopatikana kiongozi mwingine wa kushika wadhifa huo.

Kwa mjibu wa kiongozi mmoja wa Parokia ya Kanisa hilo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, hizo ni taarifa za kweli kuwa Mhashamu Askofu Mtega ametangaza kujiuzulu wadhifa huo.

Alisema hata wao hawajui kilimkuta nini maana hata hajawahi kudokeza kuhusiana na jambo hilo.

“Watumishi wote hatukujua kinachoendelea tumeshangazwa kuwa Askofu Mtega anatamka kwa kinywa chake kuwa yeye kuanzia sasa siyo Askofu Mkuu wa Jimbo hili la Songea jambo ambalo wote tulibaki midomo wazi na hatujui kuna nini,”alisema mtumishi huyo.

Baadhi ya waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Songea katika maeneo mbalimbali mjini Songea nao walionyesha kushitushwa na taarifa hizo.


Askofu huyo alilipokea jimbo hilo na kuliongoza baada ya aliyekuwa Askofu wa jimbo hilo marehemu Jacobo Komba kufariki dunia.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More