Ijumaa, 3 Mei 2013

Mei Mosi ya wafanyakazi, vipi wasio na ajira?

Tumezoea kila inapofika tarehe moja ya mwezi Mei kusherehekea siku ya wafanyakazi duniani. Siku hii hutumiwa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi nchini hasa kudai masilahi kwa Serikali.
Tunakumbuka mwaka 2010 ambapo Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta) liliandaa mgomo wa wafanyakazi likidai nyongeza za mishahara, marekebisho ya pensheni na kodi kwenye mishahara.
Mgomo ule uliiitikisa mno Serikali, kwani hata kwenye Mei Mosi ya mwaka ule, mwajiri mkuu Rais Jakaya Kikwete hakualikwa. Wafanyakazi walibaki peke yao na kujadili kero zao. Japo baadaye Rais Kikwete aliuzima mgomo huo, bado madai ya wafanyakazi yameendelea kupigwa kalenda.
Hata hivyo, katika Mei Mosi ya mwaka huu iliyofanyika jijini Mbeya juzi, Rais Kikwete ameahidi neema kwa wafanyakazi ikiwa ni pamoja na nyongeza ya mishahara na punguzo la kodi katika mishahara hiyo.
Hata hivyo, ukweli unabaki kuwa bado kuna deni kubwa kwa Watanzania walio wengi. Kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikishughulikia tu kero za watu wenye ajira ambao kimsingi ni wachache, japo hata kero zenyewe hazitatuliwi kikamilifu. Ukiangalia idadi ya wafanyakazi waliopo katika utumishi wa umma na wale wa sekta binafsi haizidi milioni moja kati ya Watanzania zaidi ya 44 milioni.
Hao ndiyo Serikali inayowatangazia neema huku kukiwa na kundi kubwa la wasio na ajira. Kati ya Watanzania milioni 44, asilimia 82 ya wenye umri wa kuajiriwa wanajishughulisha na kilimo tena cha kujikimu.
Kila mwaka kuna vijana zaidi ya 800,000 wanaomaliza shule za msingi, sekondari na vyuo wanaingia kwenye soko la ajira. Hivyo, kila mwaka kuna ongezeko la watu wasio na ajira hali inayotishia amani huko tuendako. Kwa bahati mbaya kundi hili la wasio na ajira halina mtetezi, hali chama kama vilivyo vyama vya wafanyakazi wala halina msemaji, kila mtu anakufa kivyake.
Kuna wakati ulizuka mjadala wa tatizo la ajira kwa vijana ambapo Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa alionya kuwa vijana wasio na ajira ni bomu litakalolipuka siku za usoni. Lakini kwa harakaharaka, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka aliibuka na kumjibu Lowassa akitaka orodha ya mikakati ya Serikali kwa kundi hilo. Hata hivyo, bado mikakati mingi iliyotajwa na Kabaka siyo endelevu.
Kwa mfano, muundo wa Serikali yetu haulengi kutatua tatizo la ajira kwa vijana. Mambo ya vijana yamewekwa katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na michezo. Kama kweli Serikali inalenga kuwasaidia vijana katika suala la ajira, kwa nini isiwachukue kwenye Wizara ya Kazi na Ajira?
Ninachokisema hapa ni Serikali kuweka mazingira bora kwa watu wasio na ajira ili wazipate. Ziwe rasmi au zisizo rasmi.
Kwa mfano, idadi hii kubwa ya Watanzania wanaojishughulisha na kilimo nayo itazamwe. Ni lazima kilimo hiki kirasimishwe, wakulima na wafugaji wawe na uhakika wa kupata ardhi ya kilimo na malisho. Wapate pembejeo na masoko kwa wakati.
Ukishatatua kero ya ajira kwa asilimia 82 ya wananchi, hapo angalau unaweza kupumua.
Kwa upande wa wafanyakazi nao, Mei Mosi isiwe siku ya kulilia nyongeza za mishahara, kupunguzwa kwa kodi na masuala ya pensheni peke yake. Wala siyo siku ya kumwalika Rais na kuselebuka naye jukwaani tu.
Hii inapaswa kuwa siku ya kujadili mustakabali wa kazi na maisha yetu. Kama kazi ni kipimo cha utu, uko wapi huo utu ikiwa asilimia zaidi ya 80 ya Watanzania hawana ajira za uhakika? Tukumbuke kuwa idadi hiyo ni mzigo kwa walio na ajira rasmi.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More