Ijumaa, 17 Mei 2013

Serikali yajipanga kudhibiti viroba

Dodoma. Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda amesema wizara yake itachukua hatua za haraka ili kudhibiti matumizi ya pombe zinazowekwa kwenye pakiti maarufu kwa jina la viroba ambazo zinaathiri afya za Watanzania wengi.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake bungeni Dodoma jana, Dk Kigoda alisema wizara yake itawasiliana na wadau mbalimbali ili kupata ufumbuzi wa suala hilo.
Dk Kigoda, ambaye pia ni Mbunge wa Handeni, aliwataja wadau hao kuwa ni Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara za Afya na Ustawi wa Jamii, Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Fedha na wamiliki wa viwanda vinavyotengeneza pombe hizo. “Tumelipokea suala la matumizi ya viroba kwa uzito wa hali ya juu na tutatoa uamuzi wa haraka baada ya kufanya mazungumzo na sekta mbalimbali,” alisema Dk Kigoda.
Alisema wizara yake kwa kushirikiana na wizara nyingine itatafuta njia mbadala kuepusha madhara kwa wanaotumia viroba ambavyo alisema vina athari kubwa kiuchumi na kijamii.
Alitahadharisha kuwa lazima hatua hiyo ichukuliwe kwa umakini kwani endapo vitapigwa marufuku, lazima sheria mpya ya kuzuia kinywaji hicho itungwe.
Tulichobaini
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kuhusu unywaji huo umeonyesha kuwa, idadi kubwa ya watu wanafanya kazi na kutembea wakiwa wamelewa.
Hivi karibuni imegundulika kuwa wanafunzi wengi wa shule za sekondari wamekuwa wakitumia vinywaji hivyo kwa kujificha mithili ya wavuta bangi vichochoroni.
Gazeti hili pia liligundua kuwa wanafunzi hao wanaweza kupata vinywaji hivyo kwa urahisi kwa kuwa gharama yake ni ndogo.
Imebainika kuwa wanafunzi hao wamekuwa wakifika kwenye vibanda vya wauza vocha na hata baa za vichochoroni na kutaka wauziwe vinywaji hivyo ambavyo wamevibatiza jina la juisi.
Mathalan, mmoja wa wauza vinywaji katika eneo la Gereji External, Dar es Salaam (jina linahifadhiwa) alisema wanafunzi wamekuwa wakifika dukani kwake asubuhi wakitaka viroba na kila akiwauliza husema wanakwenda kuwapa walinzi (hongo) kwa kuwa wamechelewa kufika shule.
Pombe hizo kwa sasa zinauzwa na wauza karanga, sigara na magazeti katika maeneo ya miji mikubwa nchini.
CHANZO: Mwananchi

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More