Jumanne, 28 Mei 2013

Sitta: Asema JK alinihujumu


WAZIRI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amewatuhumu viongozi wenzake ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa walishiriki kwenye njama ovu za kumnyang’anya uspika kwa sababu waliogopa spidi na viwango vyake.
Sitta alitoa kauli hiyo jana wakati alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustine (SAUT), Mwanza.
Ingawa Sitta hakuwa tayari kutaja majina ya viongozi hao waliomhujumu, ni wazi kuwa tuhuma hizo zinamwelekea moja kwa moja Rais Jakaya Kikwete, ambaye ndiye aliongoza vikao vya kupitisha jina la mgombea uspika.
Inafahamika pia kuwa Rais Kikwete ndiye aliyeleta wazo la kuwa na spika mwanamke, kigezo ambacho Sitta asingeweza kukitimiza.
Awali kabla ya kufanyika kwa vikao hivyo mwaka 2010 kulikuwa na tetesi kuwa Sitta hatakiwi kurejea kwenye kiti hicho kwa sababu alichangia kushamiri kwa upinzani na migogoro ndani ya CCM.
Baadhi ya wagombea wa CCM waliojitokeza kuchuana na Sitta katika kuwania nafasi hiyo ni Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, na Anna Makinda. Itakumbukwa kuwa wakati anagombea uspika, Sitta alikuwa ndiye Spika kwa miaka mitano iliyotangulia (2005-2010).
Alisema hujuma hiyo ililenga kumstaafisha kwa lazima kabla ya muda wake, kwa kisingizio cha wakubwa zake hao kutaka Bunge liongozwe na mwanamke, jambo ambalo alionekana kutoridhishwa nalo.
“Siku zote mimi ni mtu wa viwango na ukweli. Hata wakati nilipokuwa Spika wa Bunge, baadhi ya wakubwa zangu wa kazi hawakufurahishwa na uwazi, viwango na spidi yangu ya kuongoza Bunge.
“Kwa sababu ya baadhi ya wakubwa wangu kutofurahishwa na viwango vyangu, nilistaafishwa Uspika kabla ya muda wangu. Sababu na kisingizio chao, eti huu ni wakati wa Bunge kuongozwa na mwanamke!. Hii mmh,” alisema.
Wajuzi wa siasa ndani ya CCM wanasema kwamba hii ilikuwa mara ya pili kwa Rais Kikwete “kumhujumu” Sitta. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2005 kwa kumnyima uwaziri mkuu ambao Kikwete alikuwa amemuahidi wakati wa mchakato ndani ya kundi lake la wanamtandao.
Katika mtandao huo, Kikwete alikuwa na watu wawili aliokuwa amewaahidi uwaziri mkuu – Sitta na Edward Lowassa – kila mmoja kwa muda wake. Hata hivyo, habari za ndani zinaeleza kuwa mara baada ya kushinda, Rais Kikwete alibadili msimamo, kwa kigezo kuwa alikuwa anapata wakati mgumu kumpa uwaziri mkuu mtu ambaye (yeye Kikwete) angemmwamkia “shikamoo.”
Huo ndio ulikuwa mwanzo wa njama za kumwondoa Spika aliyekuwapo, Pius Msekwa, na kumhamasisha Sitta agombee uspika. Kundi la wanamtandao lilimpiga vita Msekwa likimwita “agano la kale,” likahakikisha Sitta anapita.
Hata hivyo, Sitta alifanya kazi ya uspika kwa msuguano mkubwa kati yake na Waziri Mkuu wa wakati ule, Edward Lowassa, ambaye alijiuzulu mwaka 2008 kwa shinikizo la Tume ya Bunge kuhusu kashfa ya kampuni tata ya kufua umeme, Richmond.
Kuhusu ufisadi, Sitta alisema amejipambanua kupambana nao pasi na woga kwakuwa anaamini hiyo ndiyo nia nzuri ya kuliokoa taifa.
Aliongeza kuwa wapo baadhi ya watu hapa nchini wanafanya biashara ya unyonyaji na wanasafirisha fedha nje ya nchi.
Alisema biashara hizo za kiunyonyaji ndizo zinazosababisha mikopo ya elimu kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kuendelea kucheleweshwa, na aliwataka wasomi na Watanzania wote kutokukubali nchi kushikwa na mafisadi, kwani watu hao ni hatari na hawana huruma na uchumi wa taifa.
“Mpaka leo hii namsifu sana Baba wa Taifa, hayati mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa uadilifu aliokuwa nao. Aliona mbali, alipiga vita ukabila na unyonyaji wa rasilimali za nchi. Hivyo, tusiruhusu tabaka la watu wanyonyaji kuongoza uchumi wa taifa hili,” alisema Sitta.
Alisema, yeye binafsi kamwe hakubaliani na vitendo vya kifisadi vinavyofanywa na baadhi ya watu, hivyo wasomi na Watanzania wasiunge mkono watu walioihujumu nchi kupitia mikataba mingi mibovu ya kifisadi.
Aidha, Waziri Sitta alieleza kusikitishwa na usiri wa mambo unaofanywa na Serikali kuhusu maendeleo ya nchi, na alitaka usiri huo usiwepo, huku akihoji: “Utaendeshaje nchi kwa usiri? Kwa nini ufanye siri kuhusu mambo ya kimaendeleo kwa wananchi wako?”
Aliponda pia kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi wa nchi unaoonekana sasa kwa kukua kwa asilimia 6.9 kwa mwaka, badala ya kukua kwa asilimia 10 hadi 12 kwa mwaka, na aliwalaumu baadhi ya viongozi nchini kutazama suala la kuongeza ajira badala ya kupigania ukuaji wa uchumi wa taifa.
Kustaafu ubunge
Alisema hivi sasa anafikiria kustaafu ubunge, na tayari ameshawaambia wapiga kura wa Urambo Mashariki juu ya azima yake hiyo.
Alisema ni vema na viongozi wengine wakafikiria kustaafu siasa baada ya kuwatumikia wananchi kwa kipindi kirefu.
“Viongozi wenzangu msipende kung’ang’ania madaraka. Nawaombeni mjifunze kusema yatosha …staafuni kama ninavyotaka kufanya mimi,” alisema.
Jitihada za kupata wasaidizi wa Rais Kikwete kuzungumzia kauli ya Sitta hazikuzaa matunda, kwani simu zao katika kitengo cha mawasiliano Ikulu, zilikuwa zimezimwa hadi tunakwenda mitamboni.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More