Ijumaa, 3 Mei 2013

Mchakato Uchaguzi TFF kurudiwa


 
Dar es Salaam. Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) limefuta mchakato wote wa uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kile ambacho kimeelezwa ni kuwapo na upungufu mkubwa na kuagiza kazi hiyo ianze upya.
Uamuzi huo ni nafuu kwa baadhi ya waliokuwa wagombea walioenguliwa na kupinga uamuzi huo kwenye uchaguzi uliojaa utata kiasi hata cha baadhi ya wagombea kukimbilia mahakamani wakiishtaki TFF, wakipinga kuenguliwa kwao.
Kabla hata ujumbe wa Fifa kutua nchini mwanzo wa mwezi uliopita kusuluhisha mgogoro huo mkubwa ndani ya TFF, Serikali kwa upande wake ilikwishaingilia kati na kuusimamisha uchaguzi huo, ikitaka kwanza kufanywa marekebisho kadhaa ya kikatiba ndipo uchaguzi huo ufanyike.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa, Fifa imebaini upungufu siyo tu namna mchakato wa uchaguzi ulivyoendeshwa, bali pia udhaifu wa vipengele kwenye katiba na kuagiza kufanywa marekebisho haraka.
Tenga alisema, Fifa wanataka kuona marekebisho yanafanywa mapema kabla ya kuanza upya mchakato wa uchaguzi, ambao agizo pia linaelekeza ufanyike kabla ya Oktoba 13.
“Kamati ya Utendaji TFF itakutana Mei 9 kwa lengo la kutoa taarifa za kuanza mchakato wa marekebisho ya katiba kama Fifa walivyoagiza katika taarifa yao kwetu,” alisema Tenga.
“Niseme tu kwamba, mchakato wa kwanza wa uchaguzi ni batili, zoezi hili linaanza upya, tena haraka iwezekanavyo. Haya ni maagizo ya Fifa,” aliongeza Tenga.
Akifafanua zaidi Tenga alisema: “Tunatakiwa kwanza kuunda kamati mbili, maadili kwa ngazi ya mwanzo na ngazi ya rufaa. Kamati hizi zitakuwa na kazi ya kushughulikia matatizo yote ya kimaadili kwa wale wote watakaokwenda kinyume na matakwa ya katiba ambayo pia Fifa imeagiza ifanyiwe marekebisho.” Aliongeza: “Kamati hizi zitasaidia kuhakikisha haki inatendeka na kuondoa migogoro kama tulivyoona awali.”
Kiini cha mgogoro huo kilikuwa ni kuenguliwa kwa wagombea wa nafasi ya makamu wa Rais, Michael Wambura na Jamal Malinzi aliyeomba urais. Wagombea hao walitua Fifa wakilalamikia kuenguliwa kwao.
Kuenguliwa kwao na wengine kadhaa kulichafua hali ya hewa, huku wadau wengi wakiitupia lawama TFF kupitia kamati zake za uchaguzi na rufaa kwa madai ya kuwapo na upendeleo wa kuwabeba baadhi ya wagombea waliodaiwa kuwa na masilahi nao.
Ujumbe wa Fifa ulikuwa nchini na kukaa siku tatu ukiwahoji baadhi ya wagombea na viongozi wa TFF na kisha kukutana na serikali na kuahidi kutoa jibu baada ya wiki moja.    

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More