Alhamisi, 2 Mei 2013

BARAZA LA MAASKOFU KATOLIKI: WANAFUNZI WATANGULIZE HEKIMA MBELE


RAIS wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, (TEC), Tarcisiuus Ngalekumtwa amewataka wanafunzi nchini kuweka hekima mbele hali itakayowasidia kuwa viongozi waadilifu katika jamii hapo baadaye.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Rais huyo, ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Iringa Mijini, wakati wa maadhimisho ya Jubilee ya kutimiza miaka 25 tangu kuasisiwa kwa shule ya Sekondari Montfort, iliyoko Rujewa mkoani Mbeya.

Akizungumza na mwanahabari wetu kwa njia ya simu, kwa niaba ya Rais huyo, Mkuu wa Shule hiyo, Ansgar Kigane, alisema Taifa lolote ili lisonge mbele kimaendeleo linahitaji kuwa na wanafunzi waliyojengeka kimaadili.

Alisema wanafunzi wa ngazi zote wanapaswa kuweka hekima mbele kitendo ambacho kitawasidia katika kumtambua mungu ambaye atawaongoza katika kutenda mema na kujiepusha na unyakuaji wa haki za wengine.

Rais Ngalekumtwa, alisistiza kuwa wanafunzi wanapaswa kuzingatia kile wanachofundishwa na wa walimu wao, lengo likiwa ni kuja kusimamia rasilimali za nchi kwa usawa na kulikomboa taifa hili kutoka kwenye dimbwi la umasikini.

Naye Mkuu wa Shule hiyo, Kigane, alisema tangu kuanzishwa shule hiyo mwaka 1988, yapo mafanikio ya kujivunia kutokana na vijana wengi waliosoma katika shule hiyo kushika nyadhifa mbambali katika baadhi ya sekta tofauti nchini.

“Shule yetu ilikuwa ikitoa elimu ya kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne lakini sasa tumepiga hatua, tunatarajia Julai mwaka huu kufungua kidato cha tano, haya nayao ni mafanikio ya kujivunia na shule yetu ni ya mchipuo wa kilimo ambacho tunakisoma kwa vitendo kutokana kuwa na mashamba ya mfano”alisema Kigane.

Alizitaja changamoto kuwa ni kushuka kwa maadili kwa pande zote, kutoka kwa wazazi na vijana ambao wengi siku hizi wamekuwa wakilelewa na mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuliko wazazi, zaidi wakishika yale machafu hali inayozidi kuchangia kushuka maadili ya vijana nchini.
Kigane alisema katika kupambana na upotofu huo shule imejipangia utaratibu wa kutoa semina kwa wanafunzi kila wiki katika madarasa yao lengo likiwa ni kuwaelimisha kuhusu faida na hasara za undawazi, ambako anaamini inaweza kuleta mabadiliko.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More