Ijumaa, 3 Mei 2013

Peter Msechu- Hivi ndivyo nilivyochukizwa na shabiki


 Dar, Tanzania. Mwanamuziki Peter Msechu anayetamba na wimbo wake mpya, ‘Kumbe’ ameeleza namna shabiki wake alivyoandika maneno ya karaha kwenye ukurasa wake wa Facebook akimhusisha mtoto wa staa huyo, Laureen.
Akizungumza na Mwananchi jana, mshindi huyo wa Tusker All Stars alisema anawapenda mashabiki wake ndio maana huwa anakubali kuwa na urafiki na mtu asiyemfahamu, lakini kitendo cha shabiki huyo kimemuudhi.
“Mtu kama huyu nimjibu nini, wasanii ndiyo wanaokufa mapema? Yeye ana uhakika wa kuishi milele? Huwa nakubali ‘friend request’ bila kuchagua ila sasa kama ndio hivi namuondoa kwenye orodha ya marafiki zangu,” alisema Msechu.
Shabiki huyo aliandika hivi kwenye ukurasa wa nyota huyo, “Sema kaka huyu ni mwanao? Kama ni mwanao hongera sana na kama si mwanao fanyafanya si unajua maisha ya wasanii ni mafupi sana.” Shabiki huyo aliandika hayo baada ya kuona picha ya binti wa staa huyo kwenye Facebook.
Msechu aliyewahi kushiriki na kushika nafasi za juu kwenye shindano la Bongo Star Search na Tusker Project Fame amesema anatarajia kufanya uzinduzi wa wimbo wake mpya huko Kigoma wiki mbili zijazo.
“Natarajia kufanya uzinduzi wa wimbo wangu kule Kigoma, ambapo nimepanga kuwa na wasanii wengine kumi na tutafanyia kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini humo,” alisema staa huyo.
CHANZO: Mwananchi

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More