Jumamosi, 4 Mei 2013

Dk Salim,Mwinyi wajipanga kulinusuru Jengo la Skauti Tz

 Dar es Salaam. Rais Mstaafu Ally Hassan Mwinyi na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) sasa Umoja wa Afrika (AU), Dk Salim Ahmed Salim wamekuwa kwenye mkakati mkali wa kulinusuru Jengo la Makao Makuu ya Chama cha Skauti Tanzania lisiuzwe.
Hatua hiyo inatokana na baada ya Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi kuamuru jengo hilo liuzwe ili kufidia deni la zaidi ya Sh111 milioni ambalo kilikuwa kinadaiwa chama hicho. Hati ya kukamatwa jengo hilo namba 1078 lililopo kiwanja namba LO 120652 ilitolewa Aprili 24, mwaka huu kupitia Kampuni ya Udalali ya Flamingo Auction Mart ambayo imetoa muda wa siku 14 fedha hiyo ilipwe au nyumba hiyo ipigwe mnada.
Gazeti hili lilitembelea ofisi za chama hicho jana na kukuta hati ya kukamatwa jengo hilo iliyosainiwa na Dalali wa Mahakama Deogratius Luziga ikiwa imebandikwa ukutani. Kwa mujibu wa hati hiyo fedha inayodaiwa ni Sh111,510,384 kupitia shauri namba 175/2009 ambapo mdai ni Agnes George aliyekuwa mfanyakazi wa chama hicho.
Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito ya chama hicho, Brigedia Jenerali Mstaafu Gerald Mkude alisema wanategemea katika kipindi cha siku 14 watashughulikia suala hilo ili kulinusuru jengo hilo lisiuzwe.
“Tulikutana na wadhamini wa chama (Mwinyi na Dk Salim) juzi na baada ya kujadiliana walitoa mapendekezo na maagizo ya kuchukua ili kuokoa jengo hilo,” alisema Mkude.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo hakuwa tayari kueleza mapendekezo hayo na kudai hawajafikia mwisho wa utekelezaji wa maagizo si rahisi kuyatamka kwa sasa.
Alisema mdai alikuwa katibu muhuktasi wa chama hicho na kwamba alilazimishwa kuacha kazi mwaka 2007 baada ya kutokea matatizo ya kiofisi.
Alisema wakati anaacha kazi madai yake yote yalikuwa ni Sh3.6 milioni lakini kutokana na sababu za kiutawala alilipwa mshahara wa mwezi mmoja tu.
Alisema hatua hiyo ilisababisha mfanyakazi huyo kuwasilisha madai yake katika Mahakama ya Kazi mwaka 2009 ambapo iliamriwa gari la chama hicho liuzwe.    

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More