Ijumaa, 17 Mei 2013

Hali si shwari Mkoani Mtwara kutokana na mgogoro wa Gesi



Vipeperushi kuhusu gesi vyatapakaa mji mzima
*RPC ataka wananchi wasihofu, ulinzi waimarishwa

CHOKOCHOKO cha ‘gesi haitoki’ zimeibuka tena mkoani Mtwara baada ya vipeperushi kusambazwa katika maeleo mbalimbali ya Manispaa ya Mtwara/Mikindani vikiwahamasisha wananchi kuhusu suala hilo.Taarifa zilizopatikana mjini Mtwara jana zilisema pamoja na vipeperushi hivyo pia umetumwa ujumbe mfupi wa simu (SMS) ukizungumzia jambo hilo.
Ujumbe uliotumwa kwenye simu na vipeperushi vilivyosambazwa vina ujumbe unaosomeka: “Kusini zinduka”, “Kusini kwanza”, “Gesi haitoki”, “Bado kilio chetu cha kupigania rasilimali yetu ipo pale pale hivyo tuungane kwa pamoja maana dhamira ya Serikali haieleweki kwa Mikoa ya kusini kama mnavyoona”.

Ujumbe huo wa simu na vipeperushi hivyo vinawahamasisha wananchi wa mkoa huo kuwa kwenye runinga na redio zao leo kusikiliza Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.

Lengo ni kujua mustakakabli msima wa gesi na kuonyesha msimmao wa wananchi hao kwa serikali.

Ujumbe huo pia unahamasisha huduma zoteza jamii kama vile maduka, masoko, daladala, bodaboda na bajaji zisimamishwe siku hiyo.

Hata hivyo kwa mujibu wa ratiba ya shughuli za Bunge mjini Dodoma, bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini inatarajiwa kuwasilishwa Jumatano ijayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Linus Sinzumwa, aliwataka wananchi wa mkoa huo kutokuwa na hofu.

Sinzumwa aliwataka waendelee na kazi zao kama kawaida na wasiogope vitisho vilivyosambazwa katika maeneo mabalimbali ya Manispaa ya Mtwara/Mikindani.

Kamanda Sinzumwa alikionya kikundi kinachosambaza ujumbe huo kuacha mara moja tabia hiyo kwa vile kufanya hivyo ni uchochezi na vurugu.

“Kuna kikundi ambacho kinasambaza ujumbe kwenye vipeperushi na kwenye simu, naomba waache mara moja kuendelea kusambaza ujumbe huo maana kufanya hivyo ni kitendo cha uchochezi, vurugu na kinyume na sheria za nchi.

“Watakaobainika wanafanya kitendo hicho ni dhahiri mkondo wa sheria utawashughulikia mara moja,” alisema na kuongeza:

“Wananchi naamini siku ya bajeti ya wizara hiyo mko huru kusikiliza ni haki yenu na kwa mujibu wa katiba ya nchi, lakini siyo kwa vitisho wala kulazimisha watu wasifanye kazi za jamii.

Siku ya bajeti ni kwa manufaa ya wananchi wote wa Tanzania na siyo ya Mtwara pekee yake…kwani bajeti nyingi za wizara zimesomwa lakini hakuna chokochoko za namna hizo zilizojitokeza.

Kamanda Sinzumwa aliwakikishia wananchi kwamba ulinzi utaimarika katika maeneo yote kwa kufanya doria za miguu na magari.

Mwishoni mwa mwaka jana zilizuka vurugu kubwa mkoani Mtwara wananchi wakipinga ujenzi wa bomba kubwa kwa ajili ya kusafirisha gesi asilia kutoka mkoani humo kwenda Dar es Salaam.

Hali hiyo ilitulia baada ya serikali kuahidi kujenga viwanda kadhaa vitakavyotumia gesi hiyo mkoani Mtwara, kikiwamo cha kusafisha gesi hiyo, licha ya gesi nyingine kusafirishwa hadi Dar es Salaam.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More