Jumamosi, 11 Mei 2013

Polisi wapiga mabomu kanisani kwa tishio la kigaidi Dar es salaam



MABOMU ya machozi yaliyopigwa kanisani na tishio la shambulio la kigaidi jana vilisababisha taharuki kwa waumini na kuvunjika kwa sala katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kunduchi Beach, jijini Dar es Salaam.
Waumini wa kanisa hilo walipatwa kiwewe baada ya bomu la machozi lililorushwa na polisi kuingia kanisani humo na baadhi ya watu kuanza kupiga kelele kufananisha hali hiyo na tukio lililotokea wiki iliyopita mkoani Arusha.
Tukio hilo lilitokea jana saa nane mchana baada ya watu wawili waliokuwa jirani na kanisa kushukiwa kutaka kufanya uhalifu hivyo baadhi ya waumini kuamua kuliarifu Jeshi la Polisi.
Awali kabla ya polisi kufika eneo hilo, ilidaiwa watu hao walilenga kulilipua kanisa hilo kama ilivyofanyika katika tukio lililotokea kwenye Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti mkoani Arusha wiki iliyopita ambapo watu watatu walifariki dunia na wengine 70 kujeruhiwa.
Baada ya polisi kupokea taarifa za kuwepo kwa watu wanaotaka kufanya uhalifu karibu na kanisa hilo la KKKT, walianza kuwashambulia wahusika kwa mabomu na risasi.
Katika mashambulizi hayo baadhi ya mabomu ya machozi yaliingia kanisani humo hali iliyowafanya waumini wataharuki huku wengine wakipiga kelele za kuomba msaada.
Purukushani hizo zilivuruga utaratibu wa sala katika kanisa hilo huku baadhi ya watu wakieneza taarifa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii kuwa kanisa hilo limelipuliwa kwa mabomu.
Taarifa hizo zilifanya baadhi ya watu katika Jiji la Dar es Salaam kuwa na wasiwasi mkubwa huku wakivilaumu vyombo vya dola kwa kushindwa kutoa ulinzi katika makanisa ambayo yanaonekana kulengwa na mashambulio ya kigaidi.
Mmoja wa waumini aliyekuwemo kanisani humo, alisema milio ya risasi na moshi wa mabomu uliokuwamo kanisani humo viliwafanya kukimbia bila uelekeo maalumu hali iliyozidisha taharuki.
“Baada ya kuhisiwa vibaya watu hao, ghafla polisi walifika eneo la tukio na kuanza kujihami ikiwemo kurusha mabomu ya machozi ambapo watu wote tuliokuwa eneo la tukio tuliamua kukimbia.
“Kiukweli tukio lile lilitufanya waumini tuchanganyikiwe sana, tungeweza kupata madhara makubwa zaidi kwa kukanyagana au kuumia kwenye viti vilivyomo kanisani,” alisema.
Malasusa agoma kuzungumza
Tanzania Daima Jumapili liliwasiliana na Kiongozi Mkuu wa KKKT nchini, Askofu Alex Malasusa juu ya kilichotokea katika moja ya makanisa yake, lakini aligoma kuzungumzia.
“Nipo kwenye mkutano, siwezi kuzungumzia jambo lolote kuhusu hilo tishio la ugaidi kama baadhi ya watu wanavyoliita,” alisema.
Kauli ya polisi
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo, alikanusha kulipuliwa kwa bomu kanisani kama baadhi ya waumini walivyodai.
Alibainisha kuwa askari polisi walifika jirani na kanisa hilo na kuanza kupambana na watu wanaosadikiwa majambazi hali iliyosababisha hofu kubwa kwa waumini waliokuwemo kanisani.
Kova alisema kuwa askari wake walikuwa kwenye doria ya kawaida ya kusaka wahalifu na ndipo lilipotokea tukio hilo la kupigwa mabomu hayo ya machozi.
Kamanda huyo aliwatoa hofu wananchi kuwa hali ya amani katika eneo hilo na Jiji la Dar es Salaam ni shwari, huku akiwasihi wazipuuze taarifa za kulipuliwa kwa Kanisa la KKKT.
“Jeshi la Polisi limejipanga kila mahali kuhakikisha vitendo kama hivyo havitokei, tumewakamata wale tuliokuwa tukiwatilia shaka,” alisema Kova.
Katika siku za hivi karibuni kumekuwa na tishio la kuvamiwa kwa makanisa mbalimbali mambo yanayochukuliwa kuwa na mlengo wa kidini.
Wiki hii Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti mkoani Arusha lilipuliwa kwa bomu ambapo watu watatu walifariki dunia na wengine 70 kujeruhiwa.
Katika tukio hilo la Arusha watu 12 hadi sasa wameshakamatwa wanne kati yao wakiwa ni raia kutoka nchini Saudi Arabia.

0 maoni:

Chapisha Maoni

Share

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More